https://youtu.be/lDuUmL5ycSY
Jina lake kamili ni Fidel Alejandro Castro Ruz. Alizaliwa tarehe 13, Augosti 1926 katika kijiji cha Birán jimbo la HolguÃn nchini Cuba. Baba yake Castro alikuwa mkulima wa miwa aliyehamia nchini Cuba akitokea Galicia, Kaskazini Magharibi mwa Hispania. Fidel Castro alikuwa mwanasiasa na mwanamapinduzi aliyeamini katika siasa za kijamaa akitumia falsafa za Karl Max na Vladimir I. Lenin. Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Cuba kati ya mwaka 1959 hadi mwaka 1976, na baadae Rais wa nchi hiyo kuanzia mwaka 1976 hadi 2008. Mnamo mwaka 2008, Castro aliamua kung'atuka madarakani kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya tumbo na kumuachia mdogo wake ajulikanae kama Rà ul Castro ambaye hadi sasa ndiye Rais wa Cuba. Castro pia aliwahi kuwa Katibu mkuu wa kwanza wa chama cha Kikomunisti cha Cuba nafasi ambayo ameitumikia kuanzia mwaka 1961 hadi 2011. Akiwa na umri wa miaka sita wazazi wake walimpeleka kwenda kuishi na mwalimu wake huko Santiago.Fidel Castro alibatizwa na kuwa muumini wa Kanisa Katoliki la Kiroma akiwa na miaka nane na kisha kujiunga na shule ya Seminari ya Bweni iitwayo La Salle iliyopo Santiago. Akiwa shuleni La Salle ,mara kwa mara Castro alionekana kuwa mtomvu wa nidhamu na hivyo ikapelekea kuhamishiwa shule ya Dolores iliyokuwa inamilikiwa na Kanisa la Kiroma huko Santiago. Baadae alihamishiwa katika shule nyingine iitwayo El Colegio de Belén mjini Havana. Ingawa shuleni alionekana kupenda zaidi masomo ya Historia na Jiografia,Castro hakufanya vizuri darasani badala yake alitumia muda wake mwingi katika michezo. Mwaka 1945 alijiunga na Chuo Kikuu cha Havana ambapo alisomea Sheria. Akiwa Chuo Kikuu Havana, Castro alionekana kupenda siasa na alikuwa mmoja wa wanaharakati wa kutetea maslahi ya wanafunzi chuoni hapo. Aliwahi pia kugombea urais wa Shirikisho la wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Havana akitumia kauli mbiu ya *uwazi,haki na usawa* lakini hakufanikiwa kushinda. Fidel Castro alikuwa akipinga mfumo wa siasa za kimagharibi (anti- imperialist) ikiwemo tabia ya Marekani kuziingilia nchi za Caribbean. Pia alionekana kupinga rushwa pamoja na uongozi mbovu wa serikali ya Cuba chini ya Rais Ramón Grau. Mnamo Novemba mwaka 1946 Castro alitoa hotuba ambayo iligonga vichwa mbali mbali vya magazeti akionesha waziwazi kutokukubalina na uongozi wa kiuonevu wa Rais Ramon Grau. Mwaka 1953 aliongoza mapinduzi ya kumng'oa madarakani aliyekuwa Rais wa Cuba wakati huo Fulgencio Batista. Hata hivyo mapinduzi hayo hayakufanikiwa na hivyo kupelekea Fidel Castro kufungwa jela. Mara baada ya kutoka jela, Castro alisafiri kwenda nchini Mexico na kuunda kikundi cha kimapinduzi kilichojulikana kama *26th of July Movement*(M-26-7) akiwa na mdogo wake Raúl Castro pamoja na mwanamapinduzi Che Guevara. Baada ya kurejea nchini Cuba akitokea Mexico, aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyopelekea kumng'oa madarakani Rais Fulgencio Batista mnamo mwaka 1959 na hatimaye kunyakua mamlaka ya kijeshi na kisiasa kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Utawala wa Fidel Castro ulipingwa vikali na Marekani ambapo ilitishia kumng'oa madarakani kwa kumuua, kumuwekea vikwazo vya kiuchumi ama kumpindua. Mara kadhaa Marekani ilikuwa ikiendesha majaribio ya kumuondoa madarakani Fidel Castro bila mafanikio yoyote. Mnamo tarehe 17, Aprili 1961 serikali ya Marekani kupitia shirika lake la kijasusi la Central Intelligence Agency (CIA) iliivamia Cuba na kutaka kumpindua Fidel Castro. Uvamizi huu ulijulikana kama *' The Bay of Pigs Invasion'*. Hata hivyo jeshi la Marekani Democratic Revolutionary Front (DRF) lililokuwa linafadhiriwa na CIA lilishindwa ndani ya Siku tatu na jeshi la Cuba ( Cuban Revolutionary Armed Forces) lililokuwa likiongozwa na Waziri Mkuu Fidel Castro. Kufuatia tishio la Marekani kutaka kumpindua Fidel Castro, Castro aliamua kuungana na U.S.S.R. ili kuweza kukabiliana ipasavyo na Marekani. Baada ya Marekani kuweka Silaha zake za Nyuklia nchini Uturuki, Fidel Castro aliamua kuwajibu kwa kuiruhusu USSR nayo kuweka Silaha za Kinyuklia nchini Cuba. Maamuzi haya yalifikiwa baada ya mazungumzo ya siri yaliyofanyika mwaka 1962 baina ya Fidel Castro na kiongozi mkuu wa USSR Nikita Khrushchev. Tukio hili linatafsiriwa kama ndilo lililochochea kuongezeka kwa uhasama kati ya Marekani na USSR na kuchochea vuguvugu la vita baridi (cold war) iliyokuwa ikiendelea kwa muda mrefu baina ya mataifa ya Kibepari yakiongozwa na Marekani na yale ya Kisoshalisti chini ya USSR. Katika uongozi wake Fidel Castrol aliifanya Cuba kuwa nchi inayofuata mfumo wa siasa za kijamaa ikiongozwa na chama kimoja cha Kikomunisti. Pia alifanya mageuzi makubwa ya kiuchumi pamoja na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu. Castro pia alimiliki vyombo vikubwa vya habari nchini Cuba na kuwadhibiti vikali wapinzani wake wa ndani na nje. Fidel Castro anachukuliwa kama kiongozi shupavu aliyeinusuru Cuba kutoka kwa ubepari wa Marekani. Amekuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi mbali mbali wa dunia kutokana na jitihada zake za kupinga ubepari. Sera za Fidel Castro zimekuwa zikiwavutia viongozi mbali mbali kama vile Hugo Chavez wa Venezuela, Evo Morales wa Bolivia, Nelson Mandela wa i,Ahmed Ben BAfrika ya Kusinella wa Algeria ,Jawaharlal Nehru wa India, n.k. Hata hivyo kwa upande wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, Fidel Castro amekuwa akichukuliwa kama kiongozi dikteta kwa kuminya Uhuru wa watu wake akifananishwa na madikteta wengine kama Adolf Hitler, Joseph Stalin,Benito Mussolini, Mao ze Dong na wengineo. Fidel Castro alianza kuumwa mwaka 2006 ambapo tarehe 31,Julai 2006 alifanyiwa upasuaji wa tumbo kufuatia utumbo wake kuvuja damu. Kufuatia hali yake kiafya kuendelea kuwa mbaya mwaka 2008 alistaafu na kumuachia urais mdogo wake Raul Castro. Tarehe 19, April 2011 alijiuzuru nafasi ya ukatibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Cuba nafasi ambayo pia ilichukuliwa na mdogo wake. Baada ya kujivua nafasi zote za uongozi ndani ya serikali ya Cuba, Castro aliendelea kuwa mshauri wa masuala
mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi ndani ya nchi hiyo. Mnamo Desemba mwaka 2014, Fidel Castro alitunukiwa tuzo ya Amani ya Confucius ijulikanayo kama Chinese Confucius
Peace Prize kutokana na jitihada zake za kutafuta suluhu ya mgogoro wa muda mrefu uliokuwa ukiendelea baina ya nchi yake na Marekani. Hatimaye Kifo chake. Taarifa zilizotolewa kupitia Television ya Taifa ya Cuba zinaeleza kwamba Fidel Castro amefariki dunia usiku wa tarehe 25,Novemba 2016 majira ya 22:29 kwa saa za Afrika ya Mashariki. Taarifa hizi zimethibitishwa na mdogo wake Raul Castro ambaye pia ndiye Rais wa nchi hiyo. Castro amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 ambapo Agosti 13 mwaka huu ndiyo ilikuwa Siku yake ya Kuzaliwa ya mwisho akiwa hapa duniani. Hata hivyo sababu za kifo chake hazikugundulika mara moja. R.I.P.......Fidel Castro!
0 Comments